Shirika
la afya duniani, WHO limearifu kuwa liko mbioni kufanya majaribio ya
chanjo dhidi ya ugonjwa wa Ebola, ambao umeripotiwa kuua takribani watu
4,500 huku nchi za Afrika Magharibi zikiripotiwa kuathirika zaidi tangu
kulipuka kwa ugonjwa huo.
Taarifa iliyoripotiwa na CNN
imesema kuwa shirika hilo limepanga kuanza utekelezaji wa jaribio hilo
mapema Januari mwaka 2015 katika nchi za Afrika Magharibi, huku
wakisisitiza kuwa chanjo zote hazina madhara kwa afya ya binadamu, japo
chanjo hiyo haitowahusu wagonjwa ambao tayari wana maambukizi Ebola.
Mratibu wa zoezi hilo Dk. Marie Paule Kieny amesema, chanjo hiyo
itatolewa kwa mtu yoyote atakayekuwa tayari kujitolea kushiriki.
Amezitaja nchi za Mali, Uingereza na Marekani kuwa ni baadhi ya nchi ambazo jaribio la chanjo hiyo litafanyika.
Shirika la afya limesema limeagiza wataalamu kufanya ziara Afrika
Magharibi katika nchi ambazo wananchi wake wameathirika zaidi na ugonjwa
huo, ambapo pia ziara hiyo itahusisha pia zoezi la ukaguzi wa vituo
ambavyo vitatumika kutolea huduma hiyo ya chanjo.
Iwapo chanjo hii itafanikiwa itafufua matumaini kwa watu wa Afrika ya
Magharibi ambao wameshuhudia athari kubwa zilizosababishwa na Ebola
ambapo watu zaidi ya 4,500 wameripotiwa kufariki na wengine zaidi ya
9,000 wana maambukizi ya ugonjwa huo.
0 comments:
Post a Comment