Followers

Sunday, 21 September 2014

 

Jina lake halisi ni Deogratius Shija na pia jina hilo hilo ndilo analofahamika nalo zaidi kwa mashabiki wake. Ni mmoja wa waigizaji wanaofanya vizuri sana kwenye tasnia ya bongo movies nchini akiwa ameshaigiza kwenye zaidi ya filamu kumi tofauti. Ni mwigizaji, mwandishi na pia mwongozaji wa filamu mwenye uwezo wa hali ya juu sana. 

PICHA AKIWA KAZINI.

  • Deogratius Shija 1

  • Deogratius Shija 2

  • Deogratius Shija 3


HISTORIA YA FAMILIA

Deogratiuos Shija alizaliwa tarehe 1 mwezi wa 12 tarehe mwaka 1978 kwenye familia yenye jumla ya watoto kumi na tano, alianza elimu yake ya msingi mkoani Tabora katika shule ya msingi Gongoni, na baadaye akahamia Dar es Salaam katika shule ya msingi Mwongozo ambako alimaliza elimu ya msingi mwaka 1992, na baadaye alirudi mkoani Tabora na kupata elimu ya sekondari katika shule ya Sekondari Uyui mjini Tabora na baada ya hapo alijiunga na Chuo cha Foradhani jijini Dar es salaam.

HISTORIA ZAMANI.

Historia ya Deogratious shija kwenye uigizaji ilianza rasmi mwaka 2000 baada ya kuacha kazi ya kuajiriwa kwenye hoteli ya White Sand jijini Dar es salaam, alipojiunga na kundi la sanaa liitwalo Malongo sanaa group lililokuwa na makazi yake maeneo ya mwananyamala, na baada ya mwaka mmoja kundi hilo liligawanyika na shija akishirikia na Mrisho Mpoto walianzisha kundi walilolipa jina la Dreams Art family ambalo malengo yake makubwa yalikuwa ni kucheza ngoma na sanaa za muziki. Baada ya kukaa na kundi hilo kwa muda, shija alipata mwaliko wa kwenda nchini uingereza kushiriki tamasha la African Caribbean Celebration mwaka 2003, na baada ya tamasha hilo kuisha aliamua kubaki nchini Uingereza kutafuta maisha ambako alikaa huko kwa takribani miaka minne na nusu na akiwa huko alifanya filamu yake ya kwanza aliyoipa jina la “Lataka moyo”, ambayo alifanya na watanzania waishio uingereza, na baadaye alifanya filamu iitwayo “Two brothers” ambayo alifanya na marehemu Juma kilowoko – Sajuki na mkewe Wastara Juma. Ambayo kwa maoni yake anasema ndiyo filamu aliyoipenda sana na ndiyo iliyomuweka juu na kumtambulisha kisanii.

Baada ya filmu hiyo alifanya filamu kama Chanzo ni mama, My book, Aisha, Imekula kwangu, Where is God na nyingine nyingi na sasa anajiandaa kuachia filamu yake mpya  ya Lazy boy.

Akizungumzia msukomo uliomsababisha aamue kujiingiza kwenye sanaa anasema kuwa alikuwa anakumbuka kipindi cha nyuma alipokuwa anaangalia maigizo na anakumbuka sana jinsi ambavyo Single Mtambalike -Richie alivyokuwa akiigiza na kumvutia na yeye kutaka kuigiza.

Akizungumzia mipango yake ya baadaye shija amesema anataka kwenda kujiendeleza kielimu zaidi kwenye upande wa uigizaji na anasubiri mambo yakae sawa ili aende. Pamoja na hilo pia shija amepanga kushiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 kwa lengo la kugombea nafasi ya ubunge kwa ajili ya kutetea wanyama na viumbe hai endapo nafasi hiyo itaruhusiwa kwenye katiba mpya inayokuja.

0 comments: