Followers

Tuesday, 28 October 2014

KISA CHA MWIZI KUIBA NA KUJISAIDIA HAJA ANAPO MALIZA WIZI WAKE

Mwizi mmoja nchini Uchina aliyekuwa na tabia ya kujisaidia haja kubwa katika nyumba anazofanywa wizi wake, hatimaye amekamatwa kutokana na teknolojia ya DNA.

Polisi jijini Cixi, katika jimbo la Zhejiang wamesema mwizi huyo aitwaye Chen mwenye umri wa miaka 29 akiwa na mwenzake walivunja nyumba moja na kuingia jikoni na kula chakula, kabla ya bwana Chen kujisaidia kwenye sakafu karibu na mlango.

Baada ya kufanya hayo, wawili hao wakaanza kutafuta vitu vya kuiba ndani ya nyumba hiyo, lakini kutokana na kukuru kakara zao, mwenye nyumba alishtuka, na wezi hao kukimbia bila ya kuiba chochote. Miezi michache baadaye, wezi hao waliingia katika nyumba nyingine na kuiba kompyuta mpakato-- yaani Laptop na fedha taslimu yuan elfu moja.

Kama kawaida, waliingia jikoni na kujipakulia chakula, na bwana chen kuacha muhuri wake wa kawaida, wa kinyesi chenye harufu kali karibu na mlango wa mbele. Mtandao wa china daily umesema polisi walifanikiwa kulinganisha vipimo vya DNA na mwizi Chen, ambaye aliwahi kutupwa gerezani kwa kosa jingine mwaka 2003. Baada ya kukamatwa, bwana Chen alikiri kujisaidia katika nyumba anazofanya wizi, akisema, amekuwa akisoma katika vitabu mbalimbali jinsi wezi wanayokuwa na mitindo yao ya kipekee, wanapofanya wizi. Polisi bado wanamsaka mwizi mwenzake.

0 comments: