Baada ya makada mbalimbali wa CCM
kutangaza nia ya kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, Mbunge wa
Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa anasema bado hajaona mtu
mwenye sifa ya kupewa nafasi hiyo kubwa nchini miongoni mwa
waliojitokeza.
Hadi sasa ni makada wa CCM pekee
waliotangaza nia hiyo ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete, wakati vyama vya
upinzani vimeingia makubaliano ya kumteua mgombea mmoja kupambana na
chama hicho tawala.
Pamoja na wanasiasa wazito wa CCM kutangaza nia
ya kugombea urais na baadhi kuanza harakati kabla ya kutangaza,
Mchungaji Msigwa anasema wote waliojitokeza hawana dira ya kuipeleka
nchi sehemu fulani kutoka hapa ilipo na hivyo hawastahili kupewa nafasi
hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mwishoni
mwa wiki iliyopita kuhusu mambo mbalimbali ya kisiasa na kijamii, Msigwa
alisema kujitangaza kwao siyo tatizo, lakini haoni kama kuna mtu mwenye
sifa za urais. “Ukimuuliza kila mmoja kwa waliojitangaza kwamba ana
vision (dira) gani kwa ajili ya nchi katika miaka mitano ijayo, wengi
watatoa ahadi badala ya kueleza ataifikisha nchi wapi katika muda huo,”
alisema mchungaji huyo bila ya kutaja majina ya waliojitokeza.
“Wengi
kati ya hawa wanaojitangaza wanataka power (madaraka) ya kulinda status
quo (nafasi zao), lakini nakuhakikishia hawana ‘vision’. Wanatumia hela
zao kununua madaraka.”
Alisema hata siku moja mti wa mwembe
haujawahi kumwita mtu akatungue maembe, bali msimu ukifika watu hufuata
mti na kutungua maembe, akimaanisha wanaojitangaza sasa hawajafuatwa na
mtu wajitangaze. “Tunahitaji mtu mwenye dira nzuri na si watu ambao
watatupa ahadi ambazo hazitekelezeki,” aliongeza mchungaji huyo wa
Iringa Vineyard Church na ambaye pia ni mratibu wa taifa wa kanisa hilo.
Pia,
Mchungaji Msigwa alisema ni wapinzani pekee ambao wana mtu ambaye ana
dira na ambaye wakati ukifika atajitokeza kutangaza kuwania kuingia
Ikulu.
“Katika Ukawa viongozi wetu wakiafikiana na tukapata mtu
mwenye maono ambaye ana anakubalika pia anaweza kupambana na mambo,
tutafanikiwa,” alisema.
Akizungumzia makubaliano ya vyama vya
upinzani kusimamisha mgombea atakayeungwa mkono na wote katika ngazi
zote kuanzia Serikali za Mitaa alisema, “Kuna tofauti kati ya mwanasiasa
na kiongozi. Mwanasiasa ni mtu anayependa kufanya mambo mazuri, lakini
kiongozi ni mtu anayefanya mambo sahihi,” aliongeza:
“Mtu anayefanya
jambo sahihi mara nyingi anafanya kwa kuwa jambo hilo linakuwa
linaumiza, lakini mtu anayefanya mambo mazuri siku zote anafurahia.
“Siasa
za siku hizi zimebadilika, hivyo mtu anayezifanya lazima ajue kwamba
kuwa mwanasiasa na kuwa kiongozi ni vitu viwili tofauti.”
Hivyo
alisema ni muhimu kwa wananchi kuwachunguza hao wanaojitangaza kuwania
urais na kuzijua tabia zao kuanzia sasa. “Ukichagua mwizi, lazima
atakwenda kuiba kwa sababu ndiyo tabia yake, hivyo ni lazima
tuwachunguze, tuwajue ili tusije kuchagua watu wenye hulka ya wizi,”
alisisitiza na kuongeza: “Tuwachunguze hawa watu na tusikurupuke.”
Vita na CCM Iringa Mjini
Akizungumzia
kauli ya viongozi wa CCM kwamba amekodishwa kiti cha Jimbo la Iringa
Mjini, Msigwa alisema: “Lugha kwamba wamenikodisha jimbo ni ya kihuni na
ni ya kupuuza. Wanavunja Katiba kwa kuwa hakuna sehemu iliyosema kwamba
jimbo ni mali ya CCM.”
Alisema ubunge wake hauna tofauti na wabunge
wengine wa majimbo kama ilivyo kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na
Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta na kwamba wananchi wa Iringa
Mjini ndiyo wanaamua nani anakuwa mbunge wao na si CCM.
“Tukiitisha
uchaguzi leo, hata CCM walete mgombea gani pale Iringa Mjini, nitamwacha
mbali sana. Nitamwacha kwa asilimia 90 kwa kuwa wamepoteana katika
jimbo kiasi kwamba wako watu 15 wanaolitaka,” alisema huku akicheka.
Alisema CCM hawaachi visingizio kwa kuwa sehemu zote Chadema iliposhinda wamekuwa wakisema walikosea uteuzi wa mgombea.
“Kwa
mfano pale kwangu huyo ambaye wanasema alikuwa na nguvu ni siasa tu za
kwenye vyombo vya habari, lakini hakuna chochote ambacho kingemfanya
ashinde 2010,” alisema Msigwa akimaanisha mgombea aliyeenguliwa kwenye
vikao vya juu vya CCM, Frederick Mwakalebela.
Katika uchaguzi huo wa
mwaka 2010, Mchungaji Msigwa alipata kura 17,740 na kumbwaga mpinzani
wake kutoka CCM, Monica Mbega ambaye alipata kura 16,914. Mbega
alishindwa na Mwakalebela kwenye kura za maoni, lakini alipitishwa na
Kamati Kuu ya CCM.
Pamoja na kushinda kwa tofauti ndogo ya kura,
Mchungaji Msigwa anasema ana uhakika wa kuendelea kuwa mbunge wa jimbo
hilo kwa kuwa amebadilisha fikra za wananchi wake kwa kuwafundisha jinsi
ya kudai haki zao.
“Kitu ambacho kitanibakiza ni jinsi
nilivyowabadilisha mtazamo wananchi wangu na hata nikiondoka leo, hilo
ndilo jambo ninalojivunia kwamba wanajitambua. Nimekuwa daraja kwa
wananchi wangu kuelewa jinsi ya kujitatulia matatizo yao,” alisema
Msigwa na kuongeza:
“Kuwapa msaada ni kitu kimoja lakini wao kujisaidia wenyewe ni jambo la muhimu zaidi.”
Hapa
Msigwa alikuwa akizungumza kwa upole na umakini kwamba wabunge wa
zamani walizoea kuwapa wananchi misaada ambayo alisema haiwezi
kuwasaidia. Hata hivyo, Msigwa anasikitika kuwa awali, alitarajia
bungeni angekutana na watu ambao wanaweza kujibu hoja anazozitoa, lakini
akakuta hali tofauti na alivyotarajia. “Yaani kwa hilo kweli
linaniumiza, watu hawajibu hoja kabisa, wanaleta siasa siasa tu. Zile
suti wengine hamna kitu kabisa,” alisema kwa sauti ya chini huku
akitingisha kichwa kuashiria kusikitika.
Katiba Mpya na Ukawa kususia Bunge
Kuhusu
uamuzi wa vyama vya upinzani vilivyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, Msigwa alisema
kitendo hicho kimefanikisha kutimiza azma yao kwa kuwa wananchi wameweza
kuelewa kwa nini walifanya hivyo.
“Tumesababisha mjadala mkubwa na
wananchi wamejifunza mengi ambayo walikuwa hawaelewi. Kitu tulichofanya
ni cha kijasiri japokuwa kuna watu wameumizwa na uamuzi huo, lakini
ujumbe umefika,” alisema.
Alisema kitendo cha polisi kuzuia
maandamano ya Ukawa katika maeneo mbalimbali nchini, kinaonyesha kuwa
CCM ilihofia matokeo ya maandamano yao katika mjadala mzima wa Katiba
Mpya.
Alisema Ukawa utafanya kazi kubwa zaidi kwenye kura ya maoni
kuhakikisha wananchi hawapigi kura ya ndiyo kwa Katiba Inayopendekezwa.
“Tutakapofika
kwenye kura ya maoni tutawaonyesha kuwa walivyocheza dansi pale
bungeni, waliwakosea wananchi. Watashindwa kwenye kura hiyo kwa kuwa
walicheza kufurahia kuwa na wabunge wasio na elimu.”
Msigwa alisema nchi iko tayari kubadilika, lakini CCM haitaki kukubali mabadiliko kwa kuwa inatumia mbinu za zamani.
Ujangili
Kuhusu
ujangili, Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii,
alisema ni tatizo nchini kwa kuwa wanaofanya biashara hiyo ni watu
wakubwa.
Alisema watu hao wengine ameshawataja, lakini bado tatizo
linaendelea hivyo ni lazima itumike njia nyingine ya kuweza kupambana na
watu hao.
“Wengine nilishawahi kuwataja na wamenifikisha mbali, nitaendelea na mapambano kuhakikisha ujangili unatokomea,” alisema.
Msigwa
alitumia nafasi hiyo kukanusha taarifa zilizokuwa zikienea kuwa amekuwa
na ugomvi na mawaziri wawili waliopita wa Wizara ya Maliasili na Utalii
akisema: “Sijawahi kuwa na ugomvi na Ezekiel Maige wala Khamis
Kagasheki kwa kuwa wajibu wangu kama kiongozi ni kusimamia yale yaliyo
sahihi.” Alisema tatizo mojawapo la mawaziri hao ni kufanya mambo kwa
siri, hivyo kuzua maswali mengi kwa watu.
“(Waziri wa sasa) Lazaro
Nyalandu yeye tunashirikiana katika kila jambo ambalo linahitaji waziri
kivuli, hiyo inatoa nafasi kuelewa mambo mengi kwa kuwa ninauona upande
wa pili, lakini akifanya makosa ninambana,” alisema Msigwa.
“Hivi
sasa kuna suala la uvunaji magogo ambalo ni tatizo kubwa, hivyo ni
lazima Nyalandu alishughulikie kwani huo ndiyo uwajibikaji.”
Uchungaji na siasa
Msigwa,
ambaye alisomea uchungaji huko Afrika Kusini, alisema kabla ya kuwa
mchungaji alikuwa mfanyabiashara wa mitumba na wakati akitekeleza
majukumu hayo, alijisikia kumtumikia Mungu kwa njia ya mahubiri.
Kutokana
na wito huo, alianza kutangaza Injili katika shule mbalimbali mkoani
Iringa huku akiendelea na biashara zake. “Baadaye nilipata nafasi ya
kwenda kusomea uchungaji Afrika Kusini na niliporudi nikawa natoa neno
la Mungu na baadaye nikaingia kwenye siasa,” alisema Msigwa.
Alisema
pamoja na kwamba yuko kwenye siasa, bado anaendelea na shughuli zake za
kichungaji kwa kuwa amejipangia muda wa kufanya hivyo.
“Napata nafasi
ya kutoa elimu kanisani, wakati mwingine ninaalikwa sehemu mbalimbali
kutoa neno na ninaendelea na siasa zangu,” alisema Msigwa.
0 comments:
Post a Comment