Baraza
la Mitihani la Tanzania (NECTA) limedhibiti na kuondoa kabisa tatizo la
wizi wa Mitihani ya Taifa na udanganyifu wakati wa Mitihani katika
ngazi mbalimbali za elimu nchini.
Mafanikio
hayo yametokana na ushirikiano uliopo kati ya NECTA na kamati za
uendeshaji mitihani katika ngazi za mikoa na wilaya ili kutatua tatizo
la wizi wa mitihani ya taifa na udanganyifu wakati wa mitihani uliokuwa
ukifanywa kinyume na taratibu za baraza la mitihani.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala wa Baraza hilo Bw.
Daniel Mafie wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jjijini Dar es
salaam uliolenga kueleza mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa.
Akifafanunua
Mafie amesema kuwa katika mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka
2013 watahimiwa waliofutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu walikuwa 13
tu ikilinganishwa na watahiniwa 9,736 waliobainika kufanya udanganyifu
mwaka 2011.
Aidha
Mafie aliongeza kuwa katika Mtihani wa Kidato cha nne mwaka 2013
watahimiwa waliofutiwa matokeo kwa kufanya udanganyifu walikuwa 272
ikilinganishwa na watahimiwa 789 mwaka 2012 na 3,303 mwaka 2011.
Akieleza
zaidi kuhusu mafanikio yaliyofikiwa Mafie alisema Baraza hilo limeweza
kusanifu mifumo ya Kompyuta yenye uwezo wa kupanga shule katika makundi
ya ubora wa ufaulu katika matokeo ya mitihani ya Taifa.
Katika
kukabiliana na tatizo la watu wanaotumia vyeti vya watu wengine au
kughushi vyeti wakati wa kuomba ajira au nafasi za masomo katika shule
mbalimbali ambapo kuanzia mwaka 2008/2009 Baraza hilo lilianzisha
utaratibu wa kuweka picha za watahimiwa katika vyeti vyao.
Katika
utaratibu huo vyeti hivyo viliwekewa alama za kiusalam hali ambayo
imesaidia Baraza hilo kuwa na uwezo wa kubaini kwa haraka na
kuwachukulia hatua wale wanaoghushi vyeti au kutumia vyeti vya watu
wengine.
Baraza
la Mitihani la Tanzania ni Taasisi ya Umma iliyochini ya Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyoanzishwa kwa sheria ya Bunge Namba 21 ya
mwaka 1973 na marekebisho yake ya mwaka 1998 na 2002 kwa ajili ya
kuendesha mitihani ya Taifa kwa lengo la kuweka misingi ya sera ya
mitihani, kuendesha mitihani na kutunuku stashahada mbalimbali na vyeti
kwa watahiniwa wanaofuzu na kufaulu mitihani iliyo chini yake kisheria.

Mkuu
wa Idara ya Fedha na Utawala wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA)
Bw. Daniel Mafie akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam
kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na Baraza hilo ikiwemo matumizi ya TEHAMA
katika usajili wa watahimiwa na uchakataji wa matokeo ya Mitihani ya
Taifa. Kulia ni Afisa Habari wa NECTA John Nchimbi.

Mkuu
wa Idara ya Fedha na Utawala wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA)
Bw. Daniel Mafie akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar s salaam
kuhusu utaratibu wa kutoa nakala za vyeti kwa watahimiwa waliopoteza
vyeti vyao ambapo utaratibu huo unahusisha uchunguzi wa uhalali wa
mwombaji. Kulia ni Afisa Habari wa NECTA John Nchimbi na kushoto ni
Msaidizi wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania Bi Glee
Magemba.

Baadhi
ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano wa Baraza la Mitihani
Tanzania (NECTA) na Vyombo vya habari uliofanyika leo jijini Dar es
salaam ukilenga kuonyesha mafanikio ya Baraza hilo nchini.(picha maelezo)
0 comments:
Post a Comment