Siasa zisiingizwe Miss Tanzania
OKTOBA 11 mwaka huu zilifanyika fainali za Shindano la Urembo
Tanzania ‘Miss Tanzania’ na kushirikisha warembo kutoka sehemu
mbalimbali hapa nchini.
Katika fainali hizo, mrembo Sitti Mtemvu alitangazwa kuwa ndiye Miss
Tanzania 2014 na kukata tiketi ya kuipeperusha bendera ya Tanzania
katika mashindano ya Dunia ‘Miss World’.
Lakini, tangu Sitti ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Temeke jijini Dar es
Salaam, Abbas Mtemvu atangazwe mshindi, wadau mbalimbali wa masuala ya
urembo walianza kupinga ushindi wake wakidai kuna upendeleo.
Mengi yamesemwa kuhusiana na ushindi huo ikiwemo madai ya kuzidi umri
uliopangwa kwa washiriki, ambao ni kuanzia miaka 18 na usizidi 24.
Katika kutetea hoja zao, wadau hao wameanika katika mitandao ya
kijamii pasi yake ya kusafiria na leseni ya gari zikionyesha ana miaka
25.
Pia wanadai siku ya shindano mrembo huyo alikiuka maelekezo baada ya
kuchagua lugha ya kiingereza katika kujibu swali lakini baadaye
akatumia Kifaransa.
Jinsi malalamiko hayo yalivyozidi, Kamati ya Miss Tanzania
imejitokeza kumtetea na kudai wao wanatambua kuwa ana miaka 23 na
alishinda kwa vigezo stahiki.
Lakini kubwa lililotusukuma Tanzania Daima kuandika tahariri hii,
jinsi baba mzazi wa Sitti, kulihusisha na masuala ya kisiasa.
Mtemvu akiwa katika majukumu yake ya kuwatumia wananchi wa jimbo lake
mwishoni mwa wiki iliyopita, aliwatuhumu watu kadhaa kuwa ndio
wanaoliratibu kwa maslahi ya kisiasa.
Mbunge alikaririwa kuwa, jambo hilo linaratibiwa mahasimu wake kisiasa ambao wana nia ya kugombea nafasi hiyo mwakani.
Sisi Tanzania Daima hatuungani na utetezi huu na kama hakuna ushahidi wa kumtetea Sitti, siasa zisitumike kama kichaka.
Mtemvu kama baba mzazi, tulitegemea aanike ukweli ikiwamo utata wa
umri wa mwanaye na si kukimbilia kuwa ni masuala ya kisiasa.
Hoja zijibiwe kwa hoja na si vinginevyo. Familia ya Mtemvu na Kamati
ya Miss Tanzania, wajipange kwa hoja na ushahidi wa uhakika ili
kurejesha imani kwa jamii ambayo ina ukakasi na ushindi wa mrembo huyo
na si kutumia siasa kichaka cha kuzima hoja za wanaodai kuna ulakini
katika ushindi wa Sitti.
0 comments:
Post a Comment