PICHA ZA UZINDUZI WA SENSA YA WATU NA MAKAZI.
Na mwandishi wetu
Ofisi ya Taifa ya Takwimu
imezindua rasmi usambazaji wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya
mwaka 2012 na kuwataka wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa wilaya na
mikoa kote nchini kuanza kutumia na kuhamasisha matumizi ya takwimu
rasmi zilizotolewa na ofisi hiyo katika kupanga mipango ya maendeleo.
Hayo yamebainishwa leo mkoani
Pwani na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa
wakati akiwakaribisha viongozi, watendaji na wadau mbalimbali wa mkoa wa
Pwani waliohudhuria semina ya usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na
Makazi ya mwaka 2012.
Amesema Tanzania ina takwimu
bora kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Ofisi yake kwa kushirikiana
na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuandaa
na kukamilisha taarifa za matokeo ya Sensa yakiwemo machapisho matatu
yanayohusu Idadi ya Watu katika ngazi ya Utawala, chapisho la Mgawanyo
wa Watu kwa umri na Jinsi na chapisho la Taarifa za Msingi za
Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi.
Dkt. Chuwa ameeleza kuwa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuhamasisha
matumizi ya takwimu za matokeo ya Sensa katika ngazi ya mkoa, wilaya na
vijiji ili ziweze kutumika katika kupanga mipango ya maendeleo.
Ameeleza kuwa takwimu
zitakazowasilishwa katika maeneo mbalimbali katinga ngazi ya kijiji,
wilaya na mikoa ukiwemo mkoa wa Pwani ambao umezindua rasmi shughuli
hiyo ya usambazaji wa matokeo zitahusu Umri, Jinsi na Viashiria muhimu
vya umri katika makundi, hali ya ndoa, hali ya uyatima na vifaa
vilivyotumika katika ujenzi wa nyumba .
Amesema lengo la usambazaji wa
takwimu hizo ni kueleza hali halisi ya mafanikio ya mikoa katika Nyanja
za uchumi, umasikini, elimu na afya ili kuwezesha uboreshaji wa maeneo
ambayo hayafanyi vizuri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Pwani Bi. Mwantumu Mahiza akizindua rasmi Usambazaji wa Matokeo ya Sensa
ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 kwa ngazi ya vijiji, Wilaya na mikoa
ameeleza kuwa usambazaji wa matokeo hayo utawasaidia na kuwarahisishia
viongozi wa maeneo mbalimbali kupanga Bajeti na mipango ya maendeleo.
Amesema matumizi ya takwimu
sahihi yatawezesha upelekaji wa huduma za jamii zikiwemo shule,
hospitali, ujenzi wa masoko, huduma za maji na kuirahisishia serikali
kuwafikishia wananchi huduma hizo kutokana na takwimu zilizoainishwa
katika maeneo husika na kuiepusha serikali kuwekeza fedha nyingi katika
miradi ambayo haiendani na idadi ya watu katika eneo husika.
Ameongeza kuwa matumizi ya
takwimu hizo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa yatasaidia kupunguza na
kuondoa migogoro ya ardhi hususani kurahisisha suala la umiliki na
mgawanyo wa ardhi kulingana na idadi ya watu na huduma.
Bi.Mahiza ametoa wito kwa
viongozi mbalimbali wa serikali na madhehebu ya dini kote nchini
kuwahamasisha wananchi kutumia takwimu zitakazosambazwa katika maeneo
mbalimbali nchini.
Naye mwakilishi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani (UNFPA) nchini
Tanzania Bw.Colins Opiyo akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo
amesema kuwa UNFPA itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha
kuwa Tanzania inakuwa na takwimu sahihi.
Amesema kuwa ili takwimu ziwe
sahihi lazima ziendane na uhalisia wa eneo husika, zitolewe katika muda
maalum , zikidhi vigezo vilivyowekwa kimataifa na kutafsiriwa kulingana
na shughuli za kiuchumi za wananchi wa Tanzania wakiwemo wakulima,
wafugaji na wafanyabiashara.
0 comments:
Post a Comment