MAMA NA WATOTO WAWILI WACHINJWA TABORA.
WIMBI
la mauaji ya kutisha limeendelea kutikisa nchini, baada ya watu
wasiojulikana kuwaua mama na watoto wake wawili kwa kuwakatakata kwa
mapanga usiku wa kuamkia juzi.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea katika Kijiji cha Nata wilayani Nzega mkoani Tabora.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, jana aliwataja waliouawa kuwa
ni mama Leticia Thomas, Marietha Nicolaus ambaye ni mwanafunzi wa darasa
la pili katika Shule ya Msingi Mwanaruru na Magreth Nicholas ambaye
umri wake haukutambulika.
“Mama
wa watoto hao aliuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga sehemu za kichwani
na bega la kushoto, hali iliyosababisha apoteze maisha hapo hapo
kutokana na majeraha mengi.
“Lakini
pia watoto Marietha na Magreth nao walikatwakatwa hivyo hivyo… mauaji
haya ni mabaya, tunaendelea na msako mkali wa kuhakikisha wahusika
wanatiwa nguvuni,” alisema Kamanda Kaganda.
Alisema
mpaka sasa chanzo cha mauaji hayo ya kinyama hakijajulikana, ingawa
kuna taarifa kuwa inawezekana yamesababishwa na masuala ya mapenzi.
“Polisi
tunaendelea na uchunguzi wetu wa kina, hatujapata chanzo cha mauaji
haya, tunaomba mtupatie muda wakati huu ambao askari wangu wanaendelea
na kazi,” alisema Kamanda Kaganda.
Alisema mpaka jana hakuna mtu hata mmoja aliyetiwa mbaroni kuhusiana na mauaji hayo.
“Kwa vile polisi tunafanya kazi zetu kisayansi, naamini tutafanikiwa ingawa mpaka sasa hakuna mtu aliyetiwa mbaroni,” alisema Kamanda.
Alisema
taarifa za kugundulika kwa miili hiyo zilitolewa na majirani ambao
walilazimika kwenda kumwangalia mama Magreth baada ya kuona amechelewa
kuamka.
“Inaonekana
baada ya tukio lile kulipopambazuka asubuhi, mama Magreth alikuwa
hajafungua mlango majirani wakaamua kwenda kugonga mlango walipoona
kimya wakaamua kuvunja mlango na kukuta familia yote imeuawa,” alisema Kamanda.
Matukio
ya watu kuchinjwa yamekuwa yakitokea kila mara ambapo Septemba 16 mwaka
huu, mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina la Melasi Ndabi aliuawa kwa
kuchinjwa na watu wanaodaiwa kufika nyumbani kwake katika Kijiji cha
Lisu wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora.
0 comments:
Post a Comment